TAMASHA LA JINSIA 2009, 8TH – 11TH 2007 “JINSIA, DEMOKRASIA NA MAENDELEO: RASILIMAlI ZIWANUFAISHE WANAWAKE WALIOKO PEMBEZONI”
Kumb: Tamasha/2009 Aprili 2009
TAMASHA LA JINSIA 2009, 8TH – 11TH 2007
“JINSIA, DEMOKRASIA NA MAENDELEO: RASILIMAlI ZIWANUFAISHE WANAWAKE WALIOKO PEMBEZONI”
Wapendwa wanaharakati, wanamtandao na marafiki wote katika vuguvugu za kupigania haki za binadamu na usawa wa kijinsia na ukombozi wa wanawake.
Kwa niaba ya Mtandao wa Mashirika Watetezi wa Haki za Binadamu, Usawa wa Kijinsia na ukombozi wa wanawake nchini Tanzania (FemAct), Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) tunayo furaha kubwa kutangaza rasmi Tamasha la Jinsia la Mwaka 2009 ambalo kwa mwaka huu litahusu Rasilimali Ziwanufaishe Wanawake Walioko Pembezoni. Mada Kuu ni Jinsia, Demokrasia na Maendeleo. Tamasha la Jinsi mwaka huu litafanyika kuanzia tarehe 8 hadi 11 Septemba 2009.
Tamasha la Jinsia ni kongamano la wanaharakati na marafiki mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi linalofanyika kila baada ya mwaka mmoja ili kutafakari, kujenga uwezo na kutandaa kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo harakati za kijinsia, ukombozi wa wanawake na haki za binadamu.
Tamasha la Jinsia 2009, ni nafasi ya wazi ya kuleta pamoja vikundi na asasi za kiraia, wanaharakati, mashirika ya utetezi, utafiti wa haki za binadamu, na wanahabari wanaojihusisha na kuunga mkono harakati mbalimbali za ushawishi na utetezi juu ya haki katika ngazi mbalimbali ikiwemo ngazi za jamii, kiwilaya, kitaifa, kikanda na kimataifa. Tamasha hili, kama yaliyopita, ni nafasi ya kukutana, kutafakari na kupanga mikakati ya baadaye au siku za usoni juu ya masuala ya haki na usawa wa kijinsia na ukombozi wa wanawake.
Tamasha la Jinsia ni nafasi ya kurejea na kutangaza historia ya wanawake katika mapambano ya ukombozi wa bara la Afrika na mapambano mengine, kujadili mafanikio, changamoto na matatizo yanayozikumba harakati za rasilimali kumnufaisha mwanamke aliyoko pembezoni. Lengo ni kuweza kuwa na msimamo wa pamoja juu ya mipango ya baadaye ya kuendeleza harakati hizi katika ngazi mbalimbali.
Malengo ya Tamasha la Jinsia 2009
- Kusisitiza na kuimarisha vuguvugu la ukombozi wa wanawake kimapinduzi, kutengeneza nafasi kwa ajili ya: kuibua, kubadilishana, na kuanzisha fikra, uchambuzi na kutengeneza mikakati ya pamoja kwenye suala la rasilimali kuweza kunufaisha wanawake walioko pembezoni;
- Kusherekea nguvu zetu za pamoja, kupanua na kuimarisha ushirikiano katika vuguvugu la kuwakomboa wanawake kimapinduzi katika ngazi na sekta zote za kijamii;
- Kuimarisha kujinoa na kuongeza uwezo wa kuchambua, kutafiti na kutathamini masuala yahusuyo Jinsia na harakati za ukombozi wa wanawake na wanyonge wengine kote duniani na
- Kuandika nyaraka na kusambatisha maarifa kuhusu harakati za ukombozi wa wanawake dunia na kuchangia kwenye mjadala wa mada kuu ya Tamasha la Jinsia 2009 na ile ya la Jinsia, Demokrasia na Maendeleo.
Mada za warsha na masuala ya yatakayo jadiliwa:
- Heshima ya Mwili na Ujinsia
- Haki za afya ya uzazi
- Ukatili dhidi ya wanawake
- Kuvunja Ukim ya kuhusu ujinsia
Kuchagua, raha na maumivu
- Haki za uchumi na maisha endelevu
- Ardhi, Madini na Misitu
- Maji
- Ajira na Maisha endelevu
- Wanaojihusisha na biashara ya ngono
- Maarifa, Sanaa na Utamaduni
- Elimu
- Utumiaji wa aina mbalimbali za uandishi na sanaa katika kujenga vuguvugu
- Lugha, Mawasiliano na Habari
- Utambuzi wa utamaduni na kuandika nyaraka za historia na kuweka kumbukumbu
- Elimu za kitamaduni na harakati za wanawake katika nganzi ya jamii
- Siasa, Uongozo na uwajibikaji
- Hatua za kimaksudi za kuwepo uwiano sawa wa kijinsia 50-50 katika ngazi zote
- Muundo wa vuguvugu, uwajibikaji katika serekali na vikundi vya kiraia
- Mijadala ya wazi ya pamoja au mtu mmoja katika jamii, vikundi na mashirika kiraia
- Wanaume katika utetezi wa haki ya usawa ya kijinisa na ukombozi wa wanawake
- Virusi Vya Ukimwi na Ukimwi: Zaidi ya Uhai
- Matatizo kutokana na utunzaji wa wagonjwa majumbani
- Haki za rasilimali
- Siasa za virusi vya ukimwi na ukimwi
Ushiriki wako/wenu unaweza kuwa katika:
- Kuandaa mada na mawasiliano mbalimbali kwa njia tofauti (sanaa, wimbo, shairi, mjadala, paneli, n.k) kwenye warsha kutokana na masuala yaliyo tajwa hapo juu;
- Kuandaa na kuratibu warsha na mijadala ya kujenga uwezo;
- Kualika na kuwezesha ushiriki mtu mmoja mmoja au vikundi kwa ajili ya kuhudhuria Tamasha;
- Kutengeneza na kufanya maonesho ya vitabu, picha, kazi za mikono n.k;
- Kuandaa maonesho ya sanaa, tumbuizo, ngoma, michezo ya kuigiza n.k;
- Ushiriki katika mijadala ya warsha na semina za Tamasha;
- Kuchangia gharama za wale watakaohudhuria, na/au waandaaji wa Tamasha.
Tafadhali wasiliana nasi mapema iwezekanavyo endapo shirika lako, kikundi chenu, au wewe mwenyewe ungependa kushiriki kwa namna yoyote ile. Tungependa kuwaweka katika ratiba za ushiriki wa Tamasha la Jinsia 2009. Ukitaka maelezo zaidi juu ya uandaaji wa mada, kisa mkasa, mchezo au maonesho, wasiliana nasi ili kupata maelezo na miongozo zaidi. Pia tunakaribisha mawazo, na ushauri juu ya namna bora zaidi ya kufanikisha Tamasha kwa mwaka 2009.
Ushiriki ni wa wazi kwa watu wote, mashiriki na vikundi vya kila aina kwa kujilipia gharama kufanikisha safari, malazi na ushiriki wenu katika Tamasha. Watu binafsi au mashirika watalipa gharama za ushiriki wao wenyewe. Tunashauri utafutaji wa fedha na vifaa mapema ili kufanikisha Tamasha hili. TGNP inaweza kusaidia kutoa barua zitakazosaidia upataji/utafutaji wa fedha kwa ushiriki wenu endapo utahitajika.
Tutafarijika sana endapo mtajiandikisha kwa wingi mapema iwezekenavyo kwa kulipa ada ya ushiriki TGNP mapema. Lugha rasmi za Tamasha ni Kiswahili na Kingereza. Tunatarajia kupata mawasiliano yenu juu ya Tamasha la Jinsia 2009 katika siku chache zijao. Unaweza kuwasiliana na waandaji wa Tamasha la Jinsia kwa kupitia info@tgnp.org (kuhusu: Tamasha la Jinsia 2009) au gf_coordinator@tgnp.org
Wenu katika harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi,
Prof. Ruth Meena, Ms. Jesca Mkuchu,
Mwenyekiti wa TGNP Mwenyekiti wa FemAct


